top of page

Zaidi ya watu 4000 hutoroka makaazi yao kila siku kufuatia mapigano nchini Burkina Faso

Shirika la UNHCR linasema kwamba mashambulizi ya mara kwa mara hufurusha watu laki saba kila mwaka.


Zaidi ya watu 4000 wanalazimishwa kutoroka makaazi yao kila siku nchini Burkina Faso. Umoja wa Mataifa unaonya kwamba visa vya mashambulizi vinazidi kuongezeka wakati ambapo makundi ya kujihami yanalenga raia wa nchi hiyo mara kwa mara.


Kufuatia kauli ya shirika la linalosaidia wakimbizi ulimwenguni, (UNHCR), zaidi ya watu 700 000 walilazimika kutoroka makwao katika kipindi cha miezi 12 iliyopita. Shirika hilo linasema kwamba takriban watu 150 000 wamelazimika kukimbilia maeneo salama katika kipindi cha wiki tatu pekee.

ree

Kulingana na UNHCR, “wanaotoroka makwao hupiga ripoti za mashambulizi katika vijiji vyao, mauaji, ubakaji na uporaji wa mali.” Kufuatia matukio haya “raia wenye hofu huacha mali yao wanapokimbilia maeneo yenye usalama.


Wengi wa waliofurushwa wamekuwa wakipewa hifadhi na jamii tofauti tofauti nchini Burkina Faso. Hata hivyo, UNHCR inasema kwamba ni vigumu kwa shirika hilo kutoa misaada kufuatia hali mbaya ya usalama inayotatiza usafiri katika maeneo mbalimbali. Hii ni kwa mujibu wa Andrej Mahecic ambaye ni msemaji wa UNHCR.


Mahecic alisisitiza kwamba hali katika kanda ya Sahel inastahili kutiliwa maanani zaidi. Msemaji huyo wa UNHCR alieleza hali hiyo kuwa janga ambalo “halifahamiki kikamilifu na limeeleweka vibaya.”

ree

Taifa la Burkina Faso linapakana na Mali upande wa kaskazini magharibi na Niger katika upande wa masharikii. Mataifa haya matatu yanayopatikana katika kanda ya Sahel yamekumbwa na hali mbaya ya usalama.


Mwezi uliopita, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulieleza baraza la usalama kwamba mashambulizi yameongezeka mara tano zaidi katika mataifa ya Burkina Faso, Mali na Niger tangu mwaka wa 2016. Kufikia mwaka 2019, zaidi ya watu 4000 wameuawa kufuatia mashambulizi hayo.


Maeneo mengi ya Sahel yanayokumbwa na mapigano ni yale ambayo hayajaendelea kwa kiasi kikubwa. Makundi mengi ya kujihami yanayoendesha oparesheni zake katika eneo la Sahel yanatumia umaskini, dini na tofauti za kikabila kama misingi ya kupata wapiganaji. Wakati huo huo, kampeni za majeshi za kukabiliana na makundi haya haramu zimekumbwa na changamoto si haba ikiwemo vifaa duni vinanyotumiwa na majeshi kukabiliana na makundi ya kigaidi. Vilevile, oparesheni za majeshi zimekumbwa na visa vya ukiukaji wa haki za kibinadamu, suala ambalo wachambuzi wanasema limechangia baadhi ya raia kujiunga na makundi ya kigaidi.

ree

UNHCR imesema kwamba zaidi ya wakimbizi 4400 kutoka Niger wamefika nchini Mali. Wakimbizi hao wametoroka msururu wa mashambulizi ya kujihami katika maeneo ya Tillaberi na Tahoa, ikiwemo mashambulizi ya mapema mwezi Januari.


Wakimbizi hao wamepata hifadhi katika miji ya Anderamboukane na Menaka ambapo walijiungana na takriban raia 7700 wa Mali waliotoroka makaazi yao kufuatia hali mbaya ya usalama.


Shirika la UNHCR limeongezea kwamba watu wengi zaidi wanazidi kuvuka mpaka kutoka Niger kuingia nchini Mali.

 
 
 

Comments


Post: Blog2_Post

Subscribe Form

Thanks for submitting!

+254 711812075

©2019 by Afrikana. Proudly created with Wix.com

bottom of page