top of page

KULA NA ADUI YAKO, LAKINI USIKUBALI AKUPAKULIE

Ishara moja ya ukomavu ni kutotaja siri za nyumbani palipo na wageni. Si kila mgeni ni mgeni,wengine majasusi. Hivyo, kadri unavyofyata ulimi wako ndipo unavyolinda maisha yako. Kuna wengi wametamka maneno kimzaha wakaishi kujuta. Wengine walinyamaza, wakaitwa waoga, lakini wakabaki hai. Anasema Robert Greene kuwa jifunze kutumia adui, maanake ni rahisi rafiki yako kukusaliti. Dhana hii ameifafanua katika kitabu chake cha sheria 48 za mamlaka.


Kabla ya kula na adui, kuna masharti ambayo yanastahili kupewa uzito. Kwanza, naijulikane kiini cha uadui maana kuna uadui wa kutofautiana tu, na kuna uadui wa paka na panya, hatima yake mmoja afe, mwingine aishi. Kimaumbile, binadamu watazozana kwa mambo mbali mbali, madogo au makubwa. Hii ni kawaida na hatima yake huwa kusameheana na kuendelea mbele.


ree


Alisema mhenga mmoja kuwa wivu hauna tiba. Nami naongeza kuwa tiba ya wivu ni kukubali kuwa kila mtu ana dhamana yake na ufanisi huja kwa wakati wake. Mojawapo ya changamoto zinazovuta Afrika nyuma ni pupa yetu ya kula minofu tulopakuliwa na mzungu. Inakuaje tunapata masalio tu ilhali rasilmali zinapatikana katika udongo wa Afrika? Mataifa ya ng'ambo hayawezi kukua kiuchumi bila Afrika. Tuna mafuta, ardhi yenye rotuba, madini aina nyingi sana, tena yenye dhamana. Hata hivyo, sisi Waafrika tunapokea misaada ya chakula, dawa, elimu, kujenga miundo msingi. Isitoshe, uchumi weti unakisiwa kukua lakini tunajua tumekopa pesa kutoka uzunguni ili kuimarisha sekta zetu.


Mwafrika adui yake mwenyewe. Alinambia Kela Indeche miaka ya hapo jadi kuwa kupiga mayowe si ishara ya kuvamiwa. Alichomaanisaha anakifahamu yeye, lakini ufahamu wangu ni kuwa vilio vyetu Afrika huwa faida ya wanaopakuliwa. Inakuaje tuwe na utajiri kuliko sehemu zote ulimwenguni alafu tulishwe na mataifa yasokuwa na chochote?


Kuna wale waliotaka kujipakulia wakanyimwa uhai. Hivi wamkumbuka Thomas Sankara wa Burkina Faso? Aliona miale ya mwafrika kujitawala na kujiongoza. Akawa kizuizi kwa mataifa ya nje kula Afrika. Akatumwa kusikorudi watu. Na Patrice Lumumba je? Aliona DRC haiwezi tena kuwa chini ya utawala wa kikoloni. Akaonekana kuwa mwiba kwenye kidonda kwa mkoloni, akakatwakatwa vipande na kuyeyushwa kwenye tindikali. Likabaki jina tu. Samora Machel naye, akambabaisha mkoloni, kifo chake kikapangwa, ndege ikaangushwa, akaaga dunia. Inashangaza sana kuwa kifo cha Samora Machel kilitangazwa siku moja kabla ya ajali ya ndege. Nkifika mbinguni nitamuuliza mwanahabari Carlos Cardosso anisimulie wapi alitoa habari hizo.


Nirejelee uadui wa Mwafrika kwa mwafrika. Ni bayana kwamba hakuna umoja Afrika. Hii ndiyo nguzo kuu anayotumia mzungu kula vyetu na kutupakulia mabaki. Professor Chihombori Quiao alipigwa kalamu na uongozi wa Muungano wa Afrika. Sababu ya kupigwa kalamu ni kufokea Ufaransa kwa kutoza kodi mataifa yalokuwa chini ya utawala wake enzi za ukoloni. Hivi, ni bora kufurahisha ufaransa na kumkandamiza mwafrika kuliko kupigania haki za mwafrika. Inasikitisha sana kuona elimu yetu imepakuliwa na mzungu. Afya yetu pia imepakuliwa na mzungu. Utawala wetu umepakuliwa na mzungu. Na sasa, madeni tuliyo nayo huenda yakawa mtego kwa vizazi vijavyo ambavyo vitakula kutoka bakuli la mzungu.


Nini maana ya elimu iwapo hatuwezi kufanya uamuzi pasi kumhusisha mzungu. Inakuaje tumekorogwa akili sana na kuona mzungu kama mungu fulani anayestahili heshima zaidi ya ndugu zetu hapa. Popote penye ishara ya umoja Afrika huwa tishio kwa mzungu. Ndo maana utapata makundi ya kujihami na ugaidi katika mataifa fulani Afrika, haswa yenye rasilmali za kuliwa. Hii isikufumbe macho, fahamu kuwa penye vurugu pana ulaji. Lakini kama kawaida, mwafrika atapakuliwa mifupa baada ya nyama kuliwa na mzungu. Na matunda ya kupakuliwa mifupa ni elimu duni, afya duni, miundo msingi duni, usalama duni, na mwafrika kusalia kuwa kituko cha dunia nusu ya karne baada ya kupata uhuru. Iwapo uhuru wetu si wa mdomo tu, basi na tukatae kupakuliwa.


 
 
 

Comments


Post: Blog2_Post

Subscribe Form

Thanks for submitting!

+254 711812075

©2019 by Afrikana. Proudly created with Wix.com

bottom of page