VYA BURE HUONDOA AKILI
- Moses Wangwa
- Oct 29, 2021
- 3 min read
Updated: Aug 28, 2022
Mtegemea cha nduguye hufa maskini. Ukijipata wewe maskini, kuna kile unachotegemea kisichokuwa chako. Sababu kuu mola kumpa kila binadamu akili zake ni ili zitumiwe kwa njia bunifu kumfaidi yeye na kizazi chake. Takwimu zinapotuonyesha asilimia kubwa ya wakenya ni maskini, fahamu kuna kile wanachotegemea. Wangekuwa majasiri hawa watafiti, wangesema wengi wetu hatutumii akili inavyostahili. Na ifahamike kuwa enzi za kutumia misuli kujikimu kimaisha zilitupa kisogo, sasa kila mtu ale kwa urefu wa kamba yake.

Kuna hatua za kuhakikisha kuwa kila mtu anatumia akili inavyostahili. Lakini wakenya tuombee serikali yetu kila saa maana ina kibarua kikubwa sana. Hivi baada ya juhudi zote kuhakikisha kuwa kila mtu amepata elimu, bado utapata watu wakienda haja barabarani. Wengine wataharibu kilichowekwa na serikali kuwapa mapato mwishowe walie serikali saidia. Tuelewane mara moja, iwapo hukuhusisha serikali ulipojiingiza kwenye noma, na usiihusishe serikali unapojipata pabaya. Kila mtu na abebe mzigo wake. Serikali itashughulikia vipi masuala ya elimu, afya na usalama kisha ishughulikie ukorofi wako wa kulewa kama samaki na kutishia majirani? Komaa.
Injili ya kuekeza imetangazwa kila mahali. Sote tuliskia tuekeza, lakini tukaelekeza rasilmali zetu palipo na tamaa zetu. Kuna mtindo wa kubeti, na una umaarufu kwa vijana wengi. Wengine wanasema ni kuekeza ila mimi nasema ni mchezo wa pata potea. Wengi wamepoteza hela nyingi tu kwa tamaa ya kuvuna wasichopanda. Wengine wakajitia kitanzi. Wengine wakavunja familia kutokana na matokeo ya betting. Cha kusikitisha zaidi, wanaoshiriki zoezi hili ni wale wa matabaka ya chini. Hivi utumie pesa zako kutabiri ushindi wa mechi, upoteze, mzungu aende kuekeza kwake kisha wewe uachwe ukipiga domo kuhusu Man U na Liverpool? Haya ni matumizi mabaya ya akili. Alafu ukijaribu kuwakosoa vijana watie bidi katika nyanja zao, wanakuuliza iwapo bidi inalipa, wapi punda tajiri? Ujeuri wa kiwango cha juu sana.
Hii ndiyo sababu yetu sisi kuvuta mkia katika mambo mengi. Sisi maskini, alafu pia tuna chembechembe za ujeuri. Kimsingi, sisi maskini wajeuri. Tunataka kwenda mawindoni bila silaha. Hatima yake, tunaanza kuibiana na kuwapiga ngeta wenzetu mitaani. Lazima tuwajibikie kila tulicho nacho maana mwindaji anayetoka mawindoni na mbuzi si mwindaji, huyo ni mwizi anayestahili kuadhibiwa.
Wengi wetu tumezoea vya bure. Ndo maana tutapigia kura wanasiasa wanaotupa pesa. Alafu niskie mtu akisema eti serikali fisadi. Si ufisadi umeanza nawe kuchukua pesa wakati wa kampeni?
Si umeuza kura yako kwa masaibu ya miaka mitano? Kenya ni yetu. Ufisadi ni wetu. Wanasiasa ni wetu. Kila uamuzi una madhara yake, alisema mzungu. Nikitafsiri: Choices have consequences. Hii tabia ya kuwa vigeugeu inaudhi sana. Heri kuelekea pabaya kuliko kutokuwa na mwelekeo maana anayeenda pabaya atarekebishwa. Tuachane na hayo. Lakini tukubali kuwa tunapenda vya bure na manufaa yake ni kula hu na hasara juu. Ukimwona mkenya wa kawaida halalamiki, jua afya yake inampa tatizo.
Mwenzangu niruhusu nikujuze maafa ya kutegemea vya bure. Moja, utakufa maskini maanake kuna methali inayosema hivyo. Wapenzi wa masomo watakwambia kuwa idadi kubwa ya watu maskini duniani wanatoka Afrika. Si eti mwafrika hajiwezi, ila anaona bora kupewa kuliko kuchapa kazi. Kuna wengi hapa Afrika wenye bidii. Lakini wachache walio na hulka ya kupata misaada ndio wanaoharibu jina. Si unajua kiazi kimoja huezosha kapu. Hivyo ndivyo ilivyo Afrika. Sasa mkoloni alituumiza kisha akatuacha; kijiografia tu lakini dhana na mikakati yake bado inatawala. Sasa tunamfuata atupe mikopo, tena kwa riba ya juu sana. Alafu miundo msingi atujengee yeye. Mawazo kama haya ndiyo yanayotuzuia kukua kiuchumi.
Kanambia mkubwa wangu kuwa anayekula bila kupiga mswaki hulalamika chakula si kitamu. Ndo maana hatuoni uzuri wa maendeleo tunayoambiwa yapo. Kuna faida gani kujengewa barabara baada ya kubomolewa makao? Kuna faida gani kuongeza vyeo uongozini wakati uongozi wenyewe hauna ushawishi? Faida ni ipi nieleze wakati fedha zinavujwa ilhali vijana hawana ajira? Majibu unayajua wewe. Sasa, kizazi changu kinakata tumaini. Ahadi zimesalia deni la miaka mingi. Wakati wa siasa, matumaini ya kupiga hatua yanafufuliwa. Baada ya siasa, matumaini hayo yanazikwa. Inakera sana kuona vijana walohitimu wakipoteza tumaini la kupata ajira. Hatuwezi kamwe kujenga taifa la Kenya pasi na kushughulikia vijana ipasavyo. Kadri tunapowatelekeza, ndivyo uhalifu unavyozidi kupanda. Inabidi wategemee vya bure maana hata viongozi wanapata utajiri kwa njia zisizoeleweka. Alafu isitoshe, ni vijana ndio wanaotumiwa kusababisha vurugu ili wafaidike wanasiasa. Kweli kutegemea vya bure kuna gharama kubwa.
Tumpe Mungu sababu za kubariki kazi zetu maana alishasema kwenye maandiko kuwa ataibariki kazi ya mikono yetu. Usingoje kupata mali kwa njia mkato. Vya bure huleta jeuri, uzembe, ufisadi na hali zote hasi kwa binadamu. Siku moja nikaelezwa kuwa iwapo bidi inalipa, nionyeshe punda tajiri. Nami nikasema kuwa maskini punda alinyimwa akili ukapewa wewe ili umtumie punda kupata utajiri. Tia bidi katika kila jambo maana mgeni siku ya tatu si mgeni tena, ni mkulima. Hatutapata misaada milele. Lini hata sisi tutatoa misaada?
Comments