Siasa 2022
- Moses Wangwa
- Oct 16, 2021
- 2 min read
Sisi ni zaidi ya wapiga kura
Vijana wa sasa fahamu hili, ni vijana wa jana ndio wanaotufanya sisi kuzozana wakati wa siasa. Si dhambi kuwa na mwanasiasa unayempendelea zaidi ya mwingine. Lakini mwanasiasa huyo anapokuchochea kumchukia mtu mwingine, hapa umebebewa akili. Matukio kama haya ya kubebewa akili hushuhudiwa mara nyingi uchaguzi unapokaribia. Wosia wangu ni huu: Kila mtu ana akili, tofauti ni matumizi. Kuwa na elimu hakumaanishi kuwa una na akili, maana kuna wengi waliohitimu kimasomo lakini matendo yao kamwe hayakwenda shule.
Hivi sasa tunaombwa kujisajili kupiga kura. Hatua hii naiunga mkono kikamilifu. Ni haki ya kila mkenya kupiga kura.

Lakini, naomba tifikirie pamoja hapa. Kuna wenzetu waliofurushwa makwao katikati ya janga la corona na katika msimu wa mvua, haki zao zilikuwa wapi? Kuna wale waliowauawa kikatili wakati wa curfew, tuseme hawakuwa na haki? Hadi sasa, wengi wa wakenya wanakosa chakula, je kuna haki kwa hawa wenzetu? Na wale wanaokosa elimu kwa kukosa karo je? Alafu vijana wanaopiga miguu kila siku kutafuta ajira bila mafanikio, pia wao wana haki? Hivi niulize, inakuaje haki ya kupiga kura kupewa uzito zaidi kuliko haki zingine za kibinadamu?
Kupiga kura bila kujua unachotaka ni matumizi mabaya ya akili. Kwa miaka mingi, wanasiasa wametupa ahadi za miundo msingi, elimu, afya maji na nyingi nyinginezo. Je, umeridhishwa na elimu hapa nchini? Na afya je? Nisemeje kuhusu usalama, barabara na ajira? Alafu niulize, nani kati ya wanasiasa wanaowania uongozi ana sera za kusuluhisha matatizo haya?

Tukiweka fikra zetu kwa hoja kama hizi, tutapata uongozi unaofaa. Tukiwa na ubinafsi, tutaishia kuumia kwa kipindi kingine cha utawala. Mhenga mmoja kanambia eti adui yako kukutawala ni sawa na kesi ya mbuzi kuamuliwa na fisi. Bado natafakari hili…
Mwanasiasa ni kondoo na mbwa mwitu kwa wakati mmoja. Hili si bonge la tusi bali ni matumizi mazuri ya lugha kama nilivyofunzwa katika shule ya upili. Mara nyingi mwanasiasa huwa mbwa mwitu. Anapoonekana kuwa kondoo, ni ngozi tu amevalia. Hapa, azimio lake huwa kutafuta kura. Anapopata uongozi anaingia mitini. Miaka mitano anatorokea Kanairo akila mapochopocho. Waliomchagua, wanasalia vitongojini wakila hu na hasara juu.
Ndo maana kasema Jackson Mandago kuwa siasa iwekwe kwenye mapafu, si moyoni. Tofauti yako na mwanasiasa ni kuwa kwake, siasa ni ya mdomo tu. Ndo maana kwa matamshi yake, wewe unamvuruga jirani. Toa siasa moyoni, tumia akiliinavyostahili usije ukasababisha maafa na chuki.

Namalizia sasa. Imeandikwa kwamba Mola hubariki kazi ya mikono yako. Pia imeandikwa kuwa mtu mzembe asipewe mlo. Hivi niulize, unanuia kula nini kwa miaka mitano ijayo? Ni kazi gani atakayobariki Maulana kwa miaka mitano ijayo? Kupiga kura ni zoezi la siku moja tu. Usiruhusu zoezi hili kukuvuta nyuma kwa miaka mitano. Wengi wetu twaombea Kenya. Maombi ni muhimu sana, na yana nafasi yake. Lakini, baada ya maombi, ni hatua gani tunazochukua? Si alisema Yakobo kuwa imani bila matendo imekufa?
Najua nimefoka sana. Nikienda zaidi ya hapo nitaharibu. Nimalizie hivi, baada ya sala, shika jembe nenda kalime maana Mungu hubariki kazi ya mikono yako wala si urefu na ufasaha wa maombi yako.
Zaidi ya siasa sote wakenya, zaidi ya siasa sote wapenda amani, zaidi ya siasa, Kenya muhimu kuliko wanasiasa.
Comments