Zaidi ya wapiganaji 30 waangamizwa na majeshi ya Ufaransa katika oparesheni nchini Mali.
- Moses Wangwa
- Feb 8, 2020
- 2 min read
Ufaransa ina majeshi 4500 katika maeneo ya Sahel na imetangaza kuongeza majeshi 600 zaidi
Majeshi ya Ufaransa yameangamiza zaidi ya wapiganaji 30 katika oparesheni ya siku mbili inayolenga makundi ya kigaidi ya ISIL na Al-Qaeda. Hii ni kwa mujibu wa majeshi ya usalama ya Ufaransa.
Nchi ya Ufaransa ambayo ilikuwa na ushawishi mkubwa wa kikoloni katika baadhi ya mataifa yaliyoko magharibi mwa Afrika ina zaidi ya majeshi 4500 katika kanda hiyo na inaendesha oparesheni Barkhane iliyoanzishwa mwaka 2014.
Wakati huo huo, umoja wa mataifa una majeshi ya kulinda usalama 13000, idadi inayoashiria kuwa hii ni mojawapo ya misheni hatari sana kufikia sasa.

Opareheni za hivi karibuni zinazoongozwa na majeshi ya Ufaransa zilifanyika Alhamisi na Ijumaa wiki hii.
Katika eneo la Gourma, wanajeshi wa Ufaransa waliwaua wapiganaji 20 na kuharibu magari kadhaa yaliyokuwa yakitumiwa na magaidi hao. Jeshi hilo linasema kuwa wapiganaji 10 zaidi waliuawa katika eneo la Liptako ambalo ndilo ngome ya kundi la ISIL. Oparesheni hizo zilihusisha ndege za vita na helikopta mbili.
Mwezi Disemba mwaka jana, majeshi ya Ufaransa yaliangamiza wapiganaji 33 nchini Mali kwa kutumia helikopta za mashambilizi na vikosi vya nchi kavu. Oparesheni hiyo iliendeshwa karibu na mpaka wa Mali na Mauritania ambapo kundi linalohusishwa na Al-Qaeda huendesha shughuli zake.

Muungano wa Mataifa na Marekani zimetumia mabilioni ya dola kutuliza hali ya usalama katika kanda ya Sahel huku mafanikio dhidi ya vita hivyo yakiwa madogo. Kanda ya Sahel imeshuhudia ongezeko la mapigano katika miezi ya hivi karibuni, suala linaloonyesha utovu wa usalama na kusababisha mamilioni ya watu kutotoka makwao.
Mwezi uliopita, ujumbe wa umoja wa mataifa katika kanda ya Afrika magharibi ulieleza baraza la usalama la umoja wa mataifa kuwa mashambulizi ya kigaidi yameongezeka mara tano katika mataifa ya Burkina Faso, Mali na Niger tangu mwaka 2016. Zaidi ya vifo 4000 viliripotiwa katika mwaka wa 2019.
Mwezi Novemba mwaka jana, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliapa kuhakiki Oparesheni Barkhane baada ya wanajeshi 13 wa Ufaransa kuaga dunia baada ya ndege zao kugongana angani.

Kufuatia mkutano wake na viongozi wa Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger hapo Januari mjini Ouagadougou, Macron aliapa kuchukua hatua za kuimarisha ushirikiano kati ya vikosi vya Ufaransa na majeshi ya mataifa hayo.
Jumapili iliyopita, Ufaransa ilisema kwamba itapeleka wanajeshi 600 zaidi katika eneo la Sahel. Kufikia sasa, wanajeshi 41 wa Ufaransa wamepoteza maisha yao katika oparesheni hiyo.
Comments