Watu 26 wauawa na kijiji kimoja kuteketezwa kufuatia shambulizi nchini Mali
- Moses Wangwa
- Jun 8, 2020
- 2 min read
Kulingana na maafisa wa serikali, shambulizi hilo lililenga kijiji kimoja cha jamii ya Fulani katika eneo tata la Mopti.
Watu 26 wameuawa na kijiji kimoja kuteketezwa katika eneo tata la Mopti lililoko katikakati mwa taifa la Mali. Hii ni kwa mujibu wa maafisa wa serikali.

Kulingana na Aly Barry ambaye ni afisa wa chama cha Tabital Pulaaku, shambulizi hilo lililenga kijiji cha Binedama kinachomilikiwa na jamii ya Fulani. Maafisa wawili zaidi wailithibitisha kisa hiki kwa wanahabari na kuongezea kuwa kijiji cha binedama kiliteketezwa na chifu wa eneo hilo kuuawa.
Afisa wa serikali katika kata ndogo ya Koro inayopatikana katika eneo la Mopti alieleza wanahabari kuwa shambulizi hilo lilitekelezwa ijumaa alasiri.
Kulingana na afisa huyo, wanawake wawili na mtoto wa miaka tisa ni miongoni mwa waliofariki.

Moulaye Guido ambaye ni Meya wa eneo jirani la Bankass linalopakana na Mopti alisema kuwa kati ya watu 20 na 30 waliuawa na washambuliaji waliokuwa wamevalia mavazi ya jeshi.
Shambulizi hili linatokea wakati ambapo visa vya ukosefu wa usalama vinazidi kuongezeka nchi Mali, raia kutoridhishwa na serikali na kuongezeka kwa visa vya dhuluma vinavyosababishwa na majeshi ya nchi hiyo.
Shambulizi hili linaongezea msururu wa mashambulizi katika kanda ya Sahel ambayo imekumbwa na ukosefu wa usalama kwa muda. Kufikia sasa, hakuna kundi lolote la kigaidi ambalo limedai kujihusisha na shambulizi hilo.

Taifa la Mali lina idadi ya raia milioni 19 na limekumbwa na visa vya uasi kuanzia mwaka 2012 wakati ambapo wapiganaji waliamuru uasi wa kujitenga wakiongozwa na jamii ya Tuareg, kaskazini mwa taifa hilo.
Mgogoro huu - ambao umesababisha vifo vya maelfu ya majeshi na raia kufikia sasa - umeenea hadi eneo la kati nchini Mali na mataifa jirani ya Burkina Faso na Niger.
Mara kwa mara, wapiganaji hushambulia kampi za kijeshi katika eneo hilo. Mapigano haya yamezua hali ya taharuki kati ya jamii jirani katika eneo hili.
Comments