Viongozi wa Muungano wa Afrika watazamia kukomesha mizozo ya kimaeneo
- Moses Wangwa
- Feb 10, 2020
- 2 min read
Baadhi ya masuala yatakayojadiliwa ni namna ya kukomesha mapigano katika nchi kama vile Libya na Sudan Kusini.
Viongozi wa mataifa na maafisa wa serikali barani Afrika wamekutana katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa kwa mazungumzo ambayo kimsingi yanalenga kukomesha mapigano katika kanda tofauti ikiwemo mataifa ya Libya na Sudan Kusini.
Kongamano la 33 la Muungano wa Afrika lilifunguliwa rasmi hapo jana katika makao makuu yaliyoko Addis Ababa chini ya mada ya mwaka 2020 ambayo ni “kunyamazisha bunduki: kujenga mazingira bora ili kukuza bara la Afrika.”

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye anamridhi rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi kama mwenyekiti wa Muungano wa Afrika alitangaza kwamba anapanga kuandaa mikutano miwili mwezi Mei: mkutano mmoja ukilenga kutatua migogoro na wa pili ukilenga kujadili maeneo huru ya kufanya biashara barani Afrika.
Rais Ramaphosa amesema kwamba uongozi wake utaelekeza juhudi katika masuala ya kutatua mizozo barani Afrika haswa katika maeneo ambayo yameshuhudia mizozo kwa kipindi kirefu. Tayari Ramaphosa ametambua Libya na Sudan Kusini kama mataifa ya kupewa kipaumbele.

Jumamosi usiku, rais Ramaphosa alikutana na rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar katika hatua yavkuleta upatanisho kati yao na ile ya ugavi wa mamlaka nchini humo. Raia wa Sudan Kusini walizama kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013 na kusababisha maelfu ya watu kuuawa.
Salva Kiir na Riek Machar wana chini ya majuma mawili kuunda serikali. Hata hivyo, wawili hao tayari wamekosa fursa mbili za kusuluhisha tofauti zao.
Katika hatua ya kukomesha mapigano nchini Libya, Muungano wa Afrika umesisitiza mara kwa mara kuhusishwa katika michakato ya amani ambayo kimsingi inaongozwa na Umoja wa Mataifa.

Katika mkutano uliofanyika mjini Brazzaville mwisho wa Januari, viongozi wa Afrika waliapa kuandaa mkutano wa maridhiano kati ya pande mbili zinazozozana nchini Libya.
Akihutubia kikao cha Muungano wa Afrika, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guturres alisema kwamba ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika ni wa umuhimu mkubwa. Guteress alisisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unaunga mkono kikamilifu mada ya Muungano wa Afrika ya kunyamazisha bunduki.
Guteress alisema kwamba “Kunyamzisha bunduki hakuhusu amani na usalama tu, bali hatua hii itakuza maendeleo ya pamoja na kulinda haki za binadamu.” Guteress alitaja changamoto tatu kuu za dharura barani Afrika ambazo ni “kumaliza umaskini, mabadiliko ya hali ya anga na kunyamazisha bunduki.”

Wakati huo huo, mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika Moussa Faki alionya kwamba “kuendelezwa kwa visa vya ugaidi kunatishia kuporomoka kwa baadhi ya mataifa ya Afrika na sharti visa hivyo viokomeshwe.”
Kikao hiki cha 33 kinatokea wakati ambapo kuna mzozo baina ya Misri na Sudan kwa upande mmoja na Ethiopia kwa upande mwingine kuhusu ujenzi wa bwawa kwenye mto Nile, suala ambalo Misri inahofia litasababisha uhaba wa maji.
Baada ya msururu wa mikutano jijini Washington, mataifa hayo matatu yalisema kwamba makubaliano ya mwisho yatatiwa sahihi mwishoni mwa mwezi huu.
Muungano wa Afrika umetangaza kwamba taifa la Kidemokrasia la Kongo ndilo litakaloridhi Afrika Kusini ifikapo mwaka wa 2021.
Comments