Somalia yatangaza hali ya dharura kufuatia uvamizi wa nzige wa jangwani
- Moses Wangwa
- Feb 2, 2020
- 2 min read
Wizara ya kilimo inasema kuwa nzige wa jangwani wanatishia mazao ya shambani nchini humo
Nchi ya Somalia ni ya kwanza kwenye eneo upembe wa Afrika kutangaza uvamizi wa nzige wa jangwani kama hali ya dharura.
Wizara ya kilimo nchi humo imesema kuwa nzige hao wanatishia usalama wa lishe katika taifa ambalo sekta ya kilimo ingali dhaifu.
Kulingana na wizara ya kilimo, “vyanzo vya chakula kwa raia wa nchi hiyo na mifugo mifugo wao viko hatarini.” Vile vile, wizara hiyo imedokeza kwamba “nzige wa jangwani hupaa kwa kimbuga kikubwa na kuharibu idadi kubwa ya mimea.

Wizara hiyo imesema kuwa hali ya dharura imetangazwa ili kuchukua hatua na kuchangisha pesa ili kukabiliana na nzige hao kabla ya kipindi cha mavuno mnamo mwezi Aprili.
Nzige wa jangwani ambao ni wenye uharibifu mkubwa husababisha uharibifu wa hali ya juu kwa mimea na kuleta visa vya njaa.
Waziri wa kilimo nchini Somalia Said Hussein Iid amesisitiza kwamba “kufuatia makali ya nzige hao, wizara yake imejizatiti kulinda hali ya lishe na maisha ya raia wa nchi hiyo.”
Waziri Hussein Iid alisisitiza kuwa iwapo hatua haitachukuliwa kwa wakati unaofaa, basi taifa la Somalia huenda likakumbwa na uhaba wa chakula.

Kulingana na kundi linalokaridia uwepo wa chakula na lishe bora, kanda ya Afrika Mashariki tayari inashuhudia kiwango cha juu cha ukosefu wa chakula huku zaidi ya watu milioni 19 wakikabiliwa na makali ya njaa.
Kulingana na shirika la Chakula na Kilimo ulimwenguni (FAO), nzige wa jangwani wamesababisha hali mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika upembe wa Afrika kwa miaka 25.
Shirika hilo linasema kuwa uvamizi wa nzige hao kwa sasa unaathiri kanda nzima ya Afrika mashariki. FAO inasisitiza kuwa iwapo hali hii haitashughulikiwa ipasavyo, huenda ikawa tauni ya nzige.
Comments