Ni sharti katiba izingatiwe, upinzani nchini Guinea wasisitiza.
- Moses Wangwa
- Jan 14, 2020
- 3 min read
Taifa la Guinea limekumbwa na visa vya maandamano makubwa ya kupinga kubalidilishwa kwa katiba tangu Oktoba mwaka jana
Serikali ya Guinea imesema kwamba itakabiliana vikali na utovu wa usalama, ikilenga mkutano wa upinzani uliopangwa kufanyika Jumatatu. Isitoshe, Serikali ya Guinea imewalaumu wapangaji wa mkutano huwa ikisema kuwa nia yao ni kupeleka nchi katika “hali isiyokuwa na mpangilio.”

Taifa hili la Afrika magharibi limekumbwa na maandamano ya kupinga hatua ya serikali kubadilisha katiba. Hofu kubwa ya upinzani ni kwamba mabadiliko ya kikatiba yatapelekea rais wa sasa Alpha Conde kuongeza kipindi chake mamlakani.
Katika usemi wake hapo Jumapili, serikali ya Guinea imeshikilia kwamba “mamlaka ya kitaifa yatatekelezwa dhidi ya wote walio na nia ya kuvuruga amani na kuwanyima raia wa Guinea uhuru wao wa kutekeleza haki zao za kimsingi”
Makundi ya upinzani yamesema kwamba yataendelea na maandamano na kuahidi kuwepo kwa maandamano makubwa Jumatatu, suala ambalo limesababisha hofu ya kuwepo kwa msururu wa makabiliano makali.
Kwa nini raia wa Guinea wanaandamana?
Kipindi cha pili cha uongozi wa Rais Alpha Conde kinamalizika mwaka huu, Makundi ya upinzani na mashirika ya haki za kibinadamu yanaghadhabika kwamba Rais Conde mwenye umri wa miaka 81 atasalia mamlakani kwa muhula wa tatu.
Mwezi jana, Rais Alpha Conde alitoa chapisho la mwongozo wa kubadilisha katiba akidai kwamba sheria za kikoloni nchini Guinea zinastahili kubadilishwa. Hata hivyo, wakosoaji wengi wanasema kwamba rais Conde anatumia hatua hiyo kama njia ya kuijuiongezea wakati ofisini kinyume na mihula miwili ya urais kama inavyoashiria katiba ya sasa.
Conde, ambaye alikuwa kiongozi wa upinzani na rais wa kwanza nchini Guinea kuchaguliwa kidemokrasia hajakakubali wala kukana madai hayo
Uchaguzi wa wabunge nchini Guinea utafanyika mwezi ujao huku uchaguzi wa urais ukifanyika baadae mwaka huu. Vilevile, kuna uwezekano wa kupiga kura za maoni katika harakati za kubadilisha katiba.
Je, maandamano yamekumbwa na vita?
Takriban watu 20 wameuawa katika makabiliano makali na vikosi vya usalama tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita. Katika maandamano ya juma lililopita kwenye mji mkuu Conakry, zaidi ya watu 12 walijeruhiwa. Mamia ya waandamanaji pia wamefungwa gerezani.

Kulingana na shirika la Human Rights Watch, sita kati ya waliofungwa gerezani ni watetezi wa haki za kibanadamu.
Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika kanda ya Magharibi ya Afrika Corinne Dufka alisema kuwa serikali ya Guinea haifai kuwanyima watu haki zao za kupinga katiba mpya.
Dufka aliongezea kwamba “kupiga marufuku maandamano, kukamatwa kwa watetezi wa haki za kibinadamu na kutumia nguvu kuwatanya waandamanaji inaonyesha kwamba serikali iko tayari kukiuka haki za kibinadamu na kunyamazisha wenye maoni tofauti.
Muungano wa Kiuchumi ECOWAS umehimiza pande zote kujadiliana ili zisuluhishe tofauti zilizoko.
Upinzani utashiriki uchaguzi?
Taifa hili lenye utajiri wa madini na idadi ya watu milioni 13 litaandaa uchaguzi wa bunge Februari 16. Hapo awali, uchaguzi ulistahili kufanyika mwishoni mwa mwaka 2018 lakini tume ya uchaguzi nchini humo ikahairisha zoezi hilo kwa sababu ambazo “hazingeweza kuepukika.”
Kufanya mambo kuwa magumu zaidi, vyama vya upinzani vimesema kuwa havitashiriki katika uchaguzi huo, Baadhi ya vyama hivyo vinatishia kuzuia uchaguzi huo usifanyike.
Kiongozi wa upinzani Cellou Dalein Diallo alisema kuwa “si suala la kutoshiriki uchaguzi tu na kutazama. Tutazuia uchaguzi huu usifanyike.”
Kulingana na katiba iliyoko sasa nchini Guinea, ili kiongozi yeyote abadilishe katiba kwa manufaa ya kuwania muhula wa tatu ofisini, kiongozi huyo anahitaji thuluthi mbili ya kura katika bunge. Kwa sasa, chama tawala cha The Rally for the Guinean People kina wingi wa wabunge, suala ambalo linarahisisha azma ya Rais Conde kubadilisha katiba.
Ushindi wa Rais Conde mwaka 2010 ulifufua matumaini ya maendeleo ya kidemokrasia nchini Guinea baada ya miongo ya udikteta. Hata hivyo, wakosoaji wa Conde wanamlaumu kwa kukandamiza wapinzani wake na kuzuia waandamanaji, jambo analopinga vikali Rais Conde.
Comments