Mashua iliyobeba wahamiaji 91 yatoweka katika bahari ya Mediterenean
- Moses Wangwa
- Feb 21, 2020
- 2 min read
Mashua moja iliyokuwa na wahamiaji 91 wengi wao wakiwa wakimbizi imetoweka katika bahari ya Mediterenean. Kulingana na kitengo cha uhamiaji katika Umoja wa Mataifa, mashua hiyo ilikuwa safarini kutoka Libya kuelekea bara Uropa.
Mashua hiyo ambayo wengi wa abiria wake ni wa asili ya kiafrika iling’oa nanga Februari tarehe nane kutoka Al-Qarbouli, eneo linalopatikana kilomita 50 mashariki mwa mji mkuu wa Libya Tripoli kuelekea Uropa.

Osman Haroun ambaye binamuye ni abiria katika mashua hiyo anasema kwamba hajaskia lolote kutoka kwa Mohamed Idris mwenye umri wa miaka 27 au marafiki zake kumi walioandamana naye katika safari hiyo.
Osman anasema kwamba kwa kawaida, yeye “hupata habari ya wanaosafiri kwa muda masaa machache tu baada ya safari kuanza.” Hata hivyo, hakuna aliyepata habari yoyote wala kuona mabaki ya mashua hiyo.
Habari za kutoweka kwa mashua hiyo zinajiri wakati ambapo kuna ukosoaji mkali kwa Muungano wa Ulaya kufuatia ukosefu wa vitengo vya uokoaji katika bahari ya Mediterenean.

Kulingana na Alarm Phone ambayo ni nambari ya dharura kwa wahamiaji wanaoitisha msaada wa uokoji baharini, kuna mabaki ya mashua yasiyoonekana vizuri katika bahari hiyo. Alarm Phone inahimiza uongozi wa Libya, Malta na Italia kupashana habari kuhusiana na shughuli za uokoaji.
Alarm Phone inasema kwamba mashua hiyo inayosemekana kusafiri kutoka Sudan, Niger, Iran na Mali iliitisha msaada wa dharura Februari tarehe tisa muda wa saa tisa unusu usiku.
Kulingana na Alarm Phone, walinzi wa pwani ya Libya walichukua muda wa masaa matano kushughukia hali hiyo baada ya kupashwa habari. Walinzi hao walituma meli mbili kwenye bahari ya Mediterenean kutafuta mashua hiyo pasi na ushahidi wowote.
Frontex, ambalo ni shirika la Umoja wa Ulaya la kulinda mipaka lilisema kwamba limetuma ndege itakayosaidia kutafuta mashua hiyo.

Tangu kutimuliwa mamlakani na kuuawa kwa aliyekuwa rais wa Libya Muammar Gaddafi mnamo mwaka wa 2011, taifa hilo limekuwa pango la walanguzi wanaowasafirisha wahamiaji kutoka bara la Afrika kuelekea pwani ya bara Uropa.
Safari ya kuelekea Uropa kwa mashua huwa na hatari nyingi. Kufikia Oktoba mwaka jana, takriban wahamiaji 19000 walikufa maji au kupotea katika safari zao kuanzia mwaka 2014.
Kwa mara nyingi, wahamiaji wengi wamelazimishwa kurudi nchini Libya na walinzi wa pwani bila kuzingatia hali ya usalama nchini humo. Mwaka huu, zaidi ya wahamiaji 1700 wamerejeshwa makwao na kuzuiliwa katika vituo mbalimbali ambako wanateswa na kudhulumiwa.
Comments