Mashambulizi nchini Burkina Faso yagharimu maisha zaidi
- Moses Wangwa
- Mar 10, 2020
- 2 min read
Zaidi ya watu 43 wauawa na sita kujeruhiwa vibaya baada ya wanamgambo kushambulia vijiji katika mkoa wa Yatenga karibu na mpaka na taifa la Mali.
Wanamgambo wasiojulikana wamewaua watu 43 katika shambulizi kwenye vijiji vilivyo kaskazini mwa Burkina Faso. Shambulizi hili linanakiliwa kama mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi katika kipindi cha mwaka mmoja katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Serikali ya Burkina Faso imesema kwamba washambuliaji hao walilenga vijiji viwili katika eneo la kaskazini karibu na mpaka wa Burkina Faso na Mali.
Kulingana na ripoti ya serikali, “shambulizi lilitekelezwa katika vijiji vya Dinguila na Barga, katika mkoa wa Yatenga mnamo jumapili”. Idadi ya waliouawa katika mkoa huo ni 43.

Majeshi yalitumwa kuwaokoa wakaaji wa vijiji hivyo na manusura sita wakapelekwa katika hospitali kupata matibabu.
Kufikia sasa, serikali ya Burkina Faso haijawekea lawama kundi lolote la kigaidi. Vilevile, hakuna kundi lolote ambalo limedai kujihusisha na shambulizi hilo.
Wanakijiji walioshambuliwa wanajulikana kuwa wafugaji wa jamii ya Fulani ambao wamekuwa wakilengwa na vikosi vya ulinzi na majeshi nchini humo kwa madai ya kuhusishwa na makundi ya kigaidi.
Burkina Faso imekabiliana na wapiganaji wanaohusishwa na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na ISIL tangu mwaka 2015. Mzozo huu umesababisha mashambulizi kwa jamii ya Fulani ambayo inasemekana kuunga mkono makundi ya wapiganaji.
Zaidi ya watu 800 wameuawa nchini Burkina Faso kuanzia mwaka 2015.

Rais wa Burkina Faso Roch Kabore amekashifu vikali shambulizi hilo na kutuma rambirambi zake kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Rais Kabore alisema haya kupitia mtandao wa Twitter.
Mauaji ya kulipiza kisasi kati ya jamii ya Fulai na jamii zingine za wafugaji yameongezeka tangu mwaka jana.
Mashambulizi mawili kaskizini mwa Burkina Faso mwezi Januari yalisababisha vifo vya watu 36 na 39. Vurugu imesababisha zaidi ya watu laki tano kutoroka makaazi yao na kufanya eneo la kaskazini kukosa uongozi dhabiti.
Wachanganuzi wanasema kwamba shambulizi la hivi karibuni linaashiria mwenendo unaoogofya.
Kulingana na William Assayo amabye ni mtafiti mkuu katika kituo cha mafunzo ya usalama, “eneo la kaskazini mwa Burkina Faso ni mojawapo ya maeneo ambayo yameshudia ongezeko la unyanyapaa dhidi ya jamii ya Fulani.”

Mwenendo wa mashambulizi pia unaonekana kutekelezwa katika taifa jirani la Mali.
Burkina Faso inapatikana katikati ya kanda ya Sahel, sehemu ambayo makundi ya kujihami yameenea kutoka Mali.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, mashambulizi nchini Mali Niger na Burkina Faso yalisababisha zaidi ya vifo 4000 mwaka 2019.
Wapiganaji wanaohusishwa na kundi la kigaidi la Al-Qaeda walisema kwamba watahudhuria majadiliano ya amani na serikali ya Mali iwapo serikali hiyo itakubali kuondoa vikosi vya usalama kutoka Ufaransa na Muungano wa Mataifa.
Hata hivyo, serikali ya Mali haijawajibu wapiganaji hao kufikia sasa. Serikali hiyo imekuwa ikipendekeza mazungumzo kwa majuma kadhaa yaliyopita ili kukomesha vurugu.
Hata hivyo, uongozi wa Mali umesema mara kwa mara kwamba unataka vikosi vya usalama kutoka Ufaransa kusalia nchini humo. Vilevile, Ufaransa iliahidi kuimarisha uwepo wa vikosi vyake katika kanda ya Sahel.
Comments