Mahakama ya Malawi yatupilia mbali uchaguzi wa rais Peter Mutharika; uchaguzi mpya kuandaliwa
- Moses Wangwa
- Feb 4, 2020
- 1 min read
Updated: Feb 5, 2020
Mahakama ya kikatiba nchini Malawi imeamrisha uchaguzi mwingine kufanyika baada ya kutupilia mbali matokea ya uchaguzi uliomrudisha mamlakani rais Peter Mutharika mwezi Mei mwaka jana. Mahakama hiyo imesema kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya udanganyifu ikiwemo kutumia vifaa vya kubadilisha maandishi katika karatasi za kupigia kura.
Rais Mutharika anakubaliwa kisheria kukata rufaa kufuatia uamuzi wa mahakama hiyo. Hata hivyo, Mutharika atasalia kuwa rais hadi uchaguzi mpya uandaliwe.

Mahakama hiyo imeamrisha uchaguzi mpya kuandaliwa kwa kipindi cha siku 150.
Kwa sasa, hali ya uongozi itasalia jinsi ilivyokuwa kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika mwezi Mei mwaka 2019.
Maandamano ya mara kwa mara yamekuwa yakishuhudiwa katika sehemu nyingi nchini humo baada ya Mutharika kutangazwa mshindi katika uchaguzi uliopita. Lazarus Chakwera, ambaye alikuwa wa pili katika uchaguzi wa urais anashikilia kwamba alinyang'anywa ushindi na akapeleka malalamishi yake mahakamani. Mutharika anasemekana kumshinda Chakwera kwa kura 159 000 pekee.
Kesi hiyo ilisababisha raia wengi wa Malawi kufuatilia matangazo ya moja kwa moja kutoka mahakamani wakati ambapo mashahidi walitoa ushahidi kuhusiana na visa vya udanganyifu. Kesi hiyo imesikizwa kwa miezi sita kabla ya uamuzi huo kutolewa.

Hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi wa urais kuamuliwa kwa njia za kisheria tangu Malawi ipate uhuru kutoka kwa serikali ya uingereza mwaka 1964.
Uamuzi wa mahakama ya Malawi ni sawia na ule wa mahakama ya Kenya iliyotupilia mbali uchaguzi wa rais Kenyatta kwa madai ya udanganyifu katika upigaji kura.
Rais Mutharika, mwenye umri wa miaka 79 amekuwa akikanusha madai ya upinzani kwamba uchaguzi mkuu ulikumbwa na visa vya udanganyifu.
Kwa kaui moja, mabalozi kutoka Uingereza, Marekani na mataifa mengine ya ulaya wamesema kwamba uamuzi wa mahakama ya Malawi ni “hatua muhimu” katika historia ya nchi hiyo.
Comments