Libya yawaachilia huru zaidi ya wafungwa 450 ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona
- Moses Wangwa
- Apr 2, 2020
- 2 min read
Tangazo hili lilitolewa na wizara ya haki baada ya watu wanane kuambukizwa ugonjwa wa Corona.
Uongozi wa Libya umetangaza kuwa utawaachilia huru zaidi ya wafungwa 450 kama mojawapo ya hatua za kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona. Kufikia sasa, watu wanane wamedhibitishwa kuwa na virusi hivyo nchini Libya.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wizara ya haki iliyotangaza kwamba maafisa wa serikali waliafikiana kuwaachilia huru wafungwa 466 kutoka kwenya vituo vya urekebishaji katika mji mkuu wa Tripoli.

Wafungwa watakaoachiliwa ni wale wanaostshili kufikishwa mahakamani au wale ambao sheria inawaruhusu kuachiliwa kwa dhamana.
Taifa hili la kaskazini mwa Afrika lilitangaza kisa cha kwanza cha virusi vya Corona Jumanne iliyopita huku muathiriwa akiwa mzee wa miaka 73 anayeripotiwa kusafiri kutoka nchini Saudi Arabia mapema mwezi Machi.
Kufikia sasa, visa vitano zaidi vya maambukizi vimeripotiwa katika mji wa Misrata ulioko magharibi mwa nchi hiyo.

Taarifa kutoka katika wizara ya haki nchini Libya inaongezea kuwa hatua zaidi “zinazolenga kupunguza msongamano kwenye jela” zitafuata agizo hili. Baaadhi ya hatua zitakazotumiwa ni pamoja na kuwasamehe wafungwa wazee, wagonjwa na wale ambao wamehudumu nusu ya kifungo chao.
Shirika la Human Rights Watch limepongeza hatua ya wizara hiyo kwa kusema kwamba ni “hatua chanya.” Hata hivyo, shirika hilo linasema kuwa uongozi wa nchi hiyo sharti ubuni mikakati zaidi ya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya COVID-19.
Katika kauli yake, Human Rights Watch inasisitiza kwamba uongozi wa Libya “unastahili kujiandaa kupunguza kuenea kwa virusi vya Corona kwenye vituo vya urekebishaji vinanvyoshuhudia msongamano wa wafungwa.” Vilevile, shirika hilo linaitaka serikali ya Libya kuwapa makaazi raia waliofurushwa makwao.

Taifa la Libya limeshuhudia machafuko tangu mwaka 2011 wakati amabapo Muamar Gaddafi alitimuliwa mamlakani.
Tangu mwezi Aprili mwaka jana, vikosi vinavyomuunga mkono Khalifa Haftar vimekuwa vikipigana ili kuumiliki mji mkuu Tripoli, hali ambayo imesababisha vifo vya mamia ya watu na kufurusha zaidi ya watu 150 000 kutoka makaazi yao.
Usemi wa shirika la kimataifa la msalaba mwekundu unaonya kwamba machafuko yanayoendelea katika sehemu nyingi nchini Libya yanatashia huduma za dharura katika maeneo yaliyo na vifaa hafifu vya matibabu.

Katika taifa la Libya, upande wa serikali unaoongozwa na serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa na upande pinzani unaotawala eneo la mashariki mwa nchi hiyo chini ya uongozi wa Haftar zimechukua hatua za kujikinga kutokana na virusi vya Corona. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kufunga shule, baadhi ya maeneo ya kibiashara, masoko na hata vituo vya afya vya kibinafsi.
Serikali tawala nchi humo imeweka muda wa kurudi nyumbani kuanza saa nane mchana hadi saa moja asubuhi. Hii inamaanisha kwamba raia wan chi hiyo wanaweza kufanya kazi zao kwa masaa sita tu kila siku.
Comments