Kuza wanawake kiuchumi ili kukomesha ukeketaji
- Moses Wangwa
- Feb 7, 2020
- 2 min read
Zaidi ya wanawake na wasichana milioni 200 huathirika kikazi na kukosa fursa za kiuchumi kufuatia ukeketaji.
Kwa mujibu wa mwanaharakati mmoja, ukeketaji wa kina dada hauwezi kamwe kukomeshwa iwapo wanawake hawatiwa moyo kukua kiuchumi. Suala hili linaibuka wakati ambapo habari kutoka umoja wa mataifa zinaonyesha kwamba huenda zoezi la ukeketaji likachukua karne kadhaa kumalizika.
Licha ya viongozi ulimwenguni kuahidi kumaliza zoezi la ukeketaji kufikia mwaka 2030, zoezi hili lingali lilivyokuwa miaka 30 iliyopita katika mataifa ya Somalia, Mali, Gambia, Guinea-Bissau, Chad na Senegal. Kulingana na Claudia Cappa ambaye ni mchanganuzi katika shirika la watoto ulimwenguni (UNICEF), “Baadhi ya mataifa hayajapiga hatua yoyote kufikia sasa, na yale yanyopiga hatua yanafanya hivyo kwa mwendo wa kinyonga”.

Inakisiwa kwamba zaidi ya wasichana na wanawake milioni 200 ulimwenguni waliopashwa tohara wanaathiriwa kiakili na kiafya kwa kiwango kikubwa. Katika kisa cha kusikitisha, msichana wa miaka 12 alifariki nchini Misri baada ya kukeketwa. Zoezi la ukeketaji lina athari kubwa kwa kuwa mara nyingi huharibu sehemu za uzazi kwa wale wanaokeketwa.
Kulingana na Jaha Dakureh, aliyeokolewa kutoka ndoa ya mapema na ukeketaji, “Azimio la kokomesha ukeketaji wa wanawake kufikia mwaka 2030 haliwezekani.” Dakureh anasisitiza kuwa, itakuwa bora zaidi iwapo watu wataekeza palipo na faida badala ya kumalizia fedha zao kwenye mashirika ya kutoa misaada.
Dakureh ambaye ni mwanzilishi wa kundi tetezi la Safe Hands for Girls anasema kwamba “Njia mwafaka ya wanawake kujisimamia na kutetea haki zao itatokana na wao kuwa na mapato zaidi.” Kundi tetezi la Safe Hands for Girls linafanya kazi katika mataifa ya Gambia, Sierra Leone na Marekani.

Vilevile, Dakureh aliwasuta wanasiasa ambao mara kwa mara wanakosa ujasiri wa kukabiliana na suala la ukeketaji na kuachia mashirika ya misaada kutekeleza wajibu huo. Anasema kwamba inasikitisha kwamba wafadhili wa kigeni mara nyingi hutoa misaada ya fedha kwa mashirika ya kimataifa yasiyoelewa tamaduni na mazoea ya watu.
Ukeketaji wa wanawake unahusishwa sana na mataifa 30 ya Afrika. Hata hivyo, shirika la UNICEF linasema kwamba ukeketaji unatekelezwa katika mataifa 50 yakiwemo yale ya bara la Asia, Mashariki ya Kati, Latin America na Mashariki ya Uropa.
Kufikia sasa, hakuna taifa lolote linalokumbwa na visa vingi vya ukeketaji lilichokua hatua kabambe za kukomesha zoezi hili kufikia mwaka 2030.
Katika mataifa yanayoathiriwa na ukeketaji wa wanawake, saba kati ya wanawake 10 wanasema kwamba zoezi hilo sharti likomeshwe. Zaidi ya nusu ya wanawake waliokeketwa wanasema kwamba wangependelea ukeketaji ukomeshwe kabisa. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa Februari tarehe sita, ambayo ni siku ya kuadhimisha vita dhidi ya ukeketaji ulimwenguni.
Shirika la UNICEF limeonyesha wasiwasi kufuatia visa vya ukeketaji vinavyohusisha wahudumu wa afya.
Kulingana na UNICEF, takriban asilimia 25 ya wasichana waliokeketwa walifanyiwa tendo hilo na madaktari, wakunga au wahudumu wa afya tofauti na hapo awali ambapo ngariba wa kitamaduni walitekeleza zoezi hilo la ukeketaji.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa UNICEF Henrietta Fore, “ukeketaji uliofanywa na daktari unasalia kuwa ukeketaji.” Henrietta alisisitiza kuwa wahudumu wa afya wanaojihusisha na ukeketaji “wanakiuka haki za kimsingi za wasichana na kusabisha madhara ya kiafya.”
Comments