Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek Machar akataa pendekezo la amani kutoka kwa Rais Salva Kiir
- Moses Wangwa
- Feb 18, 2020
- 2 min read
Kukataa kwa Riek Machar kumevunja matumaini ya kukomisha vita vya miaka sita nchini Sudan Kusini.
Waasi nchini Sudan Kusini wamekataa mpango wa amani uliopendekezwa na rais Salva Kiir. Mpango huo wa amani unalenga kupunguza idadi ya majimbo na kubuni maeneo matatu ya kuendeshea shughuli za serikali.
Uamuzi wa Riek Machar kupinga mapendekezo hayo umevunja matumaini ya kukomesha mapigano nchini humo ambayo yamesababisha vifo vya watu 380 000 na kuwaacha mamilioni kwenye lindi la umaskini.

Salva Kiir na Riek Machar wamekuwa chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa mataifa mbalimbali kusuluhisha tofauti zao kabla ya tarehe 22 Februari.
Mnamo Jumamosi, rais Salva Kiir alisema kwamba taifa la Sudan Kusini litagawanywa na kuwa na majimbo kumi kama unavyopendekeza upande wa Riek Machar, na kuongezea maeneo matatu zaidi ya kuendesha shughuli za serikali ambayo ni Pibor, Ruweng na Abyei.
Kwa upande wake, Riek Machar alisema kwamba aliridhishwa na uamuzi wa serikali kupunguza idadi ya majimbo hadi kumi. Hata hivyo, Machar hakuridhishwa na hatua ya serikali kubuni maeneo matatu zaidi ya kuendeshea shughuli zake.

Akizungumza na vyombo vya habari, Riek Machar alisema kwamba uamuzi wa serikali haukubaliki kamwe kwa kuwa hauzingatii mapendekezo ya wafuasi wake kikamilifu.
Machar alisema kwamba upande wake “unahimiza serikali kuangalia tena suala la kuongeza maeneo zaidi ya kutekeleza shughuli za serikali.” Alionya kwamba maeneo ya Pibor, Ruweng na Abyei yanatishia kuongeza changamoto zaidi katika uongozi wa taifa hilo.
Taifa la Sudan Kusini lilikuwa na majimbo kumi kama ilivyonakiliwa kwenye katiba yake wakati lilipopata uhuru kutoka kwa taifa la Sudan mwaka 2011.
Hata hivyo, rais Salva Kiir aliongeza idadi ya majimbo hadi 28 kufikia mwaka 2015, na baadaye kuongeza majimbo zaidi na kufikia jumla ya majimbo 32.
Rais Salva Kiir alisema kwamba uamuzi wa kurudia majimbo kumi kama ilivyokuwa hapo awali ulikuwa uamuzi mgumu lakini ni uamuzi unaofaa mradi tu amani ipatikane nchini humo. Kiir alitoa amri ya kuwaachisha kazi magavana wote 32 mnamo jumamosi.

Vile vile, Salva Kiir alisema kwamba mswada wa majimbo utajadiliwa kikamilifu punde tu serikali ya muungano itakapobumiwa.
Utajiri wa mafuta unachangia sehemu kubwa ya mapato ya Sudan Kusini, na kufanya taifa hilo kuwa miongoni mwa mataifa yanayotegemea mafuta sana ulimwenguni.
Kati ya maeneo matatu mapya yaliyopendekezwa, moja wapo ni eneo tata la Ruweng lililoko kaskazini mwa nchi hiyo na lenye utajiri wa mafuta.
Eneo la Ruweng limeshuhudia mapigano makali kati ya jamii ya Dinka ambayo ni jamii ya rais Salva Kiir na ile ya Nuer anakotoka kiongozi wa waasi Riek Machar.
Shinikizo kutoka kwa Marekani na mataifa mengine imekuwa kubwa huku mataifa hayo yakisisitiza kwamba Kiir na Machar waungane na kuunda serikali ya mpito kabla ya tarehe 22 Februari.
Itakumbukwa kwamba wapinzani hawa wawili walikubaliana kuweka mkataba wa amani mwaka wa 2018 baada ya shinikizo kutoka kwa umoja wa mataifa, Marekani na mataifa jirani.
Comments