Idadi ya waliofariki kutokana na homa ya Lassa nchini Nigeria yafika sabini
- Moses Wangwa
- Feb 14, 2020
- 2 min read
Maafisa wa afya wanashuku visa vilivyoripotiwa vimeongezeka kutoka 700 hadi 1708 huku taifa hilo likikabiliana na janga hilo.
Maafisa wa afya nchini Nigeria wamesema kwamba idadi ya watu walioaga dunia nchini humo kutokana na homa ya Lassa imeongezeka na kufikia 70, huku visa vilivyothibitishwa vikiongezeka.
Kituo cha kukabiliana na magonjwa nchini Nigeria kimeripoti vifo nane zaidi vilivyosabaishwa na homa hiyo kwa kipindi cha majuma matatu.
Kulingana na kituo hicho, wahudumu wanne wa afya waliathiriwa katika majimbo ya Ondo, Delta na Kaduna.

Vilevile, kituo hicho cha kukabiliana na magonjwa kimesema kwamba visa vinavyoshukiwa vimeongezeka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na visa vya mwezi Januari. Idadi ya visa vya homa hiyo inakisiwa kuongezeka kutoka 700 hadi 1708.
Binadamu huambukizwa homa ya Lassa kupitia chakula au vifaa vya nyumbani vilivyochafuliwa na mkojo au kinyesi cha panya.
Baadhi ya dalili za homa ya Lassa ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa, vidonda vya midomo, kuumwa na misuli, kuvuja damu chini ya ngozi na kufeli kwa moyo na figo.
Kulingana na shirika la afya ulimwenguni WHO, dawa za kutibu homa ya Lassa zinaonekana kuwa na ufanisi “iwapo zitatumiwa katika hatua za kwanza za homa hiyo.”
Taifa la Nigeria ambalo lina idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika lina maabara tano zilizo na uwezo wa kugundua ugonjwa huo.

Homa ya Lassa imewekwa kwenye kundi moja na ugonjwa hatari wa Ebola na virusi vya Maburg.
Homa ya Lassa mara nyingi inapatikana nchini Nigeria na ilipata jina hilo kutoka mji wa Lassa ulioko kaskazini mwa Nigeria ambapo homa hii iligunduliwa mwaka 1969.
Kulingana na kituo cha kuzuia na kukabiliana ma magonjwa nchini Marekani, homa ya Lassa huathiri kati ya watu 100 000 na 300 000 kila mwaka na kusababisha takriban vifo 5000.
Hapo awali, visa vya homa hii vimeripotiwa katika mataifa ya Sierra Leone, Togo na Benin.
Idadi ya visa vinavyoripotiwa huongezeka mwezi wa Januari kufuatia hali ya anga katika msimu wa ukame.
Comments