Hali tata yazidi kushuhudiwa kaskazini mwa Mozambique
- Moses Wangwa
- Nov 14, 2020
- 2 min read
Umoja wa mataifa umesikitishwa na ongezeko la visa vya mapigano kaskazini mwa Mozambique
Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kutafuta mbinu za haraka za kulinda raia katika mkoa wa Cabo Delgado kaskazini mwa Mozambique huku ukionya kuwa raia wako katika hali tatanishi.
Afisi ya kushughulikia haki za kibidadamu katika umoja wa mataifa imesema kwamba mashambulizi kutoka kwa makundi ya kujihami yameongezeka katika eneo hilo katika kipindi cha wiki za hivi karibuni na kusababisha vifo vya makumi ya watu mbali na kuwafurusha wengine.

“Waliosalia kwenye mkoa hawana mahitaji ya kimsingi na wanakumbwa na athari za kuuawa, kunyanyaswa kijinsia, kushikwa mateka au kulazimishwa kujiunga na makundi ya kujihami.”
Makundi ya kujihami yamesababisha maafa mkoani Cabo Delgado kwa miaka mitatu sasa, kwa kushambulia vijiji na miji kama mojawapo ya kampeni za kuanzisha serikali huru.
Washambuliaji hao wameboresha mbinu zao katika miezi ya hivi karibuni na wametumia nguvu kunyakua wilaya kubwa; hali ambayo imesababisha maafa makubwa kwa raia.

Katika kipindi cha majuma mawili, kumekuwa na msururu wa mashambulizi katika vijiji tofauti. Walioshuhudia walisema kwamba makaazi ya raia na majengo ya umma yaliteketezwa na watu kadhaa kuuawa.
Juma lililopita, washambuliaji waliwaua wanaume na wavulana 12 waliokuwa wakishiriki sherehe za tohara.
Machafuko katika eneo hilo yamesababisha vifo vya watu 2000 tangu mwaka 2017. Takwimu za shirika moja la utafiti wa mizozo ya kujihami nchini Marekani zinaonyesha kwamba zaidi ya nusu ya waliouawa ni raia.
Zaidi ya watu laki nne wamefurushwa makwao kufuatia mgogoro huo na kutafuta makao katika miji inayopatikana karibu.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 14000 wametorokea Pemba, mji mkuu katika mkoa huo katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja.

Maelfu ya raia wanaaminika kujificha vichakani katika sehemu za mapigano. Hii ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Bachelet amesisitiza kwamba “ni sharti serikali iwalinde raia walioko ndani na nje ya maeneo yaliyoathirika.” Vilevile, Bachelet ameagiza serikali ya Mozambique kulinda mashirika ya misaada yanayotoa usaidizi kwa walioathirika.”
Kamishna huyo wa haki za kibinadamu alisema kuwa hatua hii ni muhimu haswa kufuatia athari za ugonjwa wa kipindupindu na kuenea kwa virusi vya COVID-19. Mkoa wa Cabo Delgado ni mojawapo ya sehemu zilizoathirika sana na virusi vya COVID-19 nchini Mozambique.
Umoja wa Mataifa umesema kwamba umepokea ripoti kuhusu ukiukaji unaetekelezwa na vikosi vya usalama ikiwemo mauaji. Bachelet ameagiza kwamba madai hayo yafanyiwe uchunguzi na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Comments